Вход на сайт

Просмотр новости

Найдите то, что Вас интересует

Minyukano Inavyozima ndoto za upinzani kushika dola

Дата публикации: 28-07-2026 19:53:05

Soma zaidi hapa...

Основное содержимое страницы с новостью.

By  Juma Issihaka

News Reporter

Mwananchi Communicatinons Ltd

Minyukano Inavyozima ndoto za upinzani kushika dola

Wakati vyama vya upinzani vikijinasibu kuwa nguzo ya demokrasia na taasisi za kuisimamia Serikali, hali ya uhusiano miongoni mwao inawatia mashaka baadhi ya wachambuzi wa siasa nchini.

Mashaka ya wachambuzi hao, yanatokana na mfululizo wa mabishano na hali ya kutupiana maneno miongoni mwa viongozi wa vyama vya upinzani, wakisema pengine hawajui wanayemnufaisha.

Katika miezi ya karibuni, viongozi wa vyama vya upinzani wamekuwa wakirushiana lawama hadharani, kutofautiana kuhusu mikakati ya kisiasa na hata kutuhumiana, jambo ambalo linatajwa kuwarudisha nyuma katika mapambano yao.

Julai 10, 2026, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema ACT Wazalendo kimesaliti damu za Watanzania kwa kusaini tamko la pamoja kuingia kwenye maridhiano kati yake na CCM visiwani Zanzibar.

“ACT Wazalendo imeamua kwa mara nyingine tena kusaliti harakati za mabadiliko,” alisema Mnyika, katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Siku iliyofuata, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita alimjibu Mnyika akisema anashangazwa na kauli yake huku akikitaka chama hicho kitafute wasaliti ndani yao badala ya kuishambulia ACT-Wazalendo.

Alisema mara kadhaa wamekuwa wakiiandikia Chadema na vyama vingine vya upinzani kuomba waungane katika mapambano ya demokrasia, lakini chama hicho huwa hakijibu wala kutoa ushirikiano.

Mbali na hilo, Mnyika huyohuyo, Juni 3, mwaka huu, katika mkutano wa hadhara Kilwa Kivinje, alisema Maalim Seif Sharif Hamad aliwahi kujuta kujiunga na ACT Wazalendo.

“Kati ya mambo Maalim Seif aliwahi kuyajutia sana na sisi tumezungumza naye alikuwa anafunguka, anasema sana ni kwamba alifanya kosa wakati wa kutoka CUF kwenda ACT Wazalendo,” alisema.

Kauli hizo ni sehemu ya mfululizo wa tofauti zinazoshuhudiwa zikijitokeza kwa vyama vya upinzani, hali inayowafanya baadhi ya wadau kuhoji iwapo migogoro hiyo inajenga au inabomoa harakati za kisiasa zinazolenga kuleta mabadiliko.

Katika historia ya Tanzania, muungano wa vyama vya upinzani nchini, umewahi kufanyika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na uliundwa Ukawa.

Muungano huo, uliundwa na Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD. Vyama vyote hivyo, viliweka mgombea mmoja wa urais, Edward Lowassa na kugawana majimbo ili kuepuka kugawana kura za upinzani.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kamati ya Uangalizi wa Uchaguzi Tanzania (Temco) mwaka 2016, vyama vilivyokuwa ndani ya Ukawa vilishinda jumla ya majimbo 68 kati ya 264.

Chadema kilishinda majimbo 35, CUF majimbo 32 na NCCR-Mageuzi jimbo moja. Kwa pamoja Ukawa ilipata wabunge 68 wa majimbo, sawa na takribani asilimia 26 ya majimbo yote.

Hata mgombea urais Lowassa, alipata asilimia 40 ya kura zote, ushindi ambao ni mkubwa zaidi kuwahi kupatikana kwa vyama vya upinzani tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1992.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Chadema kilipata majimbo 23 pekee, lakini mwaka 2015 baada ya kuundwa kwa Ukawa.

Athari za migogoro

Akizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa, Dk Victor Allan anasema jambo la kwanza kuathirika ni imani ya wananchi kwa vyama vinavyotarajiwa kuwa mbadala wa uongozi.

Anasema wananchi wengi hawafuatilii kwa undani tofauti za kimkakati zilizopo ndani ya vyama vya upinzani, bali wanatazama uwezo wa viongozi kuonyesha mshikamano katika masuala yenye maslahi ya umma.

“Mwananchi wa kawaida anapotazama siasa huwa anajiuliza nani ana suluhisho la matatizo yake. Akiona viongozi wanatumia muda mwingi kushambuliana, anaanza kuhoji kama wanaweza kushirikiana kutatua changamoto za Taifa,” anasema.

Dk Allan anasema siasa ni mchezo wa kujenga matumaini na kuaminika. Taswira ya migogoro ya kudumu huathiri uwezo wa vyama kuwashawishi watu ambao hawana uamuzi wa moja kwa moja wa kisiasa.

“Kila chama kinapomshambulia mwenzake, kuna sehemu ya wananchi wanaopoteza hamasa. Wengine wanaona hakuna tofauti kubwa ya kile wanachoambiwa na kile wanachokiona kwenye vitendo,” anasema.

Anasema anayenufaika kwa hatua ya kwanza ni mpinzani wa vyama vinavyogombana kwa sababu huonekana hana shinikizo kubwa kutoka kwa kambi ambayo inapaswa kuelekeza nguvu kwake.

Anasema nguvu inayotumika kujibu mashambulizi ya kisiasa kati ya vyama vya upinzani ingeweza kutumika kueleza sera, kuhamasisha wapigakura na kujenga ushawishi.

Mchambuzi mwingine, Profesa Baraka Mfinanga anasema migogoro hiyo inaathiri zaidi uwezo wa upinzani kujenga ajenda ya pamoja kuhusu masuala makubwa ya kitaifa.

Anasema katika mifumo mingi ya kidemokrasia duniani, vyama vinaweza kutofautiana katika mbinu lakini vikakubaliana katika mambo makubwa yanayogusa maslahi ya wananchi.

“Changamoto inaanza pale chama kinapoanza kuona chama kingine cha upinzani kama adui kuliko mshindani wake wa kisiasa. Hapo nguvu za harakati zinaanza kugawanyika,” anasema.

Anasema wapigakura wengi hawavutiwi na migogoro ya viongozi bali wanataka kusikia majibu ya changamoto za maisha yao ya kila siku.

“Wananchi wanapambana na gharama za maisha, ajira na huduma za jamii. Wakiona mijadala mingi inahusu nani ni msaliti na nani si msaliti, wanaweza kuona vipaumbele vimepotea,” anasema.

Profesa Mfinanga anasema migogoro ya muda mrefu pia inajenga mazingira ya kutoaminiana hata miongoni mwa wanachama wa ngazi za chini.

Anasema hali hiyo inaweza kufanya hata pale kunapotokea haja ya kushirikiana katika jambo fulani la kitaifa, msingi wa kuaminiana unakuwa umeharibika.

Mifano kutoka mataifa mengine ya Afrika imekuwa ikitajwa mara kwa mara katika mjadala wa umuhimu wa ushirikiano wa kisiasa.

Nchini Kenya, mwaka 2002, vyama mbalimbali vya upinzani viliungana kupitia muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) na kufanikiwa kuiondoa madarakani Kanu iliyokuwa imetawala kwa miongo kadhaa.

Huko Zambia, uchaguzi wa mwaka 2021 ulishuhudia Hakainde Hichilema akiingia madarakani baada ya kupata uungwaji mkono kutoka makundi mbalimbali ya kisiasa yaliyokuwa yakitaka mabadiliko ya uongozi.

Senegal nayo ilishuhudia nguvu ya mshikamano wa kisiasa wakati kambi ya upinzani ilipofanikiwa kushinda uchaguzi wa urais wa mwaka 2024.

Ingawa mazingira ya kisiasa ya kila nchi ni tofauti, mifano hiyo inaonyesha namna ushirikiano wa kisiasa unavyoweza kuongeza ushindani na kuimarisha ushawishi wa vyama vinavyolenga kupata madaraka.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa na utawala, Dk Sofia Kambona anasema madhara huonekana katika eneo la uhamasishaji wafuasi hasa nyakati za upigaji kura.

Anasema kundi kubwa la wapiga kura huwa halijafungamana moja kwa moja na chama chochote, hivyo huamua kulingana na taswira wanayoiona kwa viongozi wa kisiasa.

"Unaweza kutofautiana leo, lakini mazingira ya kisiasa yanaweza kukulazimisha kushirikiana kesho. Ndiyo maana lugha za kisiasa zinahitaji kutolewa kwa tahadhari," anasema.

Dk Sophia anasema kila kauli kali inayotolewa hadharani inaacha kumbukumbu inayoweza kutumiwa baadaye na wapinzani wa kisiasa.

Anasema mara nyingi wananchi wanakumbuka migogoro mikubwa kwa muda mrefu kuliko hata sera ambazo zilikuwa zinajadiliwa wakati huo.

Nani ananufaika?

Mchambuzi mwingine wa siasa, Said Majjid anasema swali la nani ananufaika lina majibu zaidi ya moja, lakini mnufaika mkuu huwa ni yule ambaye hashambuliwi moja kwa moja.

Anasema katika mazingira ambayo vyama vya upinzani vinaelekezea mashambulizi kwa kiwango kikubwa, shinikizo kwa wapinzani wao wa kisiasa unapungua.

“Kisiasa, unapomfanya mwenzako wa karibu kuwa lengo kuu la mashambulizi, unampunguzia mzigo yule ambaye ulipaswa kushindana naye mbele ya wananchi,” anasema.

Anasema migogoro hiyo pia huathiri wananchi wanaotamani kuona sauti mbadala yenye nguvu katika kusukuma ajenda za uwajibikaji na mageuzi.

“Demokrasia yenye afya inahitaji upinzani wenye nguvu na unaoaminika. Vyama vinaposhindwa kusimamia tofauti zao, wananchi wanaweza kupoteza imani kwa mfumo mzima wa ushindani wa kisiasa,” anasema.

Majjid anasema tofauti za kisiasa si tatizo, bali namna zinavyosimamiwa ndiyo huamua kama zitakuwa chanzo cha nguvu au chanzo cha udhaifu.

Migogoro isiwe ajenda

Mtaalamu wa sayansi ya siasa, Dk Baraka Mtemi, anasema migogoro ndani ya vyama vya upinzani ni jambo linaloweza kutokea katika mfumo wowote wa kisiasa, lakini changamoto ni pale inapogeuka kuwa jambo linalotawala ajenda kuliko hoja za msingi.

Kwa mtazamo wake, migogoro hiyo mara nyingi humsaidia mtawala wa kisiasa kwa sababu huondoa nguvu ya pamoja ya vyama vinavyopaswa kuisimamia Serikali.

“Upinzani unapopoteza muda mwingi kujadili tofauti zao kuliko sera zao, wananchi huanza kupoteza imani na uwezo wao wa kuleta mabadiliko,” anasema Dk Mtemi.

Vyama vya upinzani, anasema vina nafasi katika demokrasia kwa sababu vinapaswa kuwa jicho la wananchi na kutoa mbadala wa uongozi.

Lakini pale viongozi wanaposhambuliana hadharani, kutuhumiana au kugombania nafasi za kisiasa, anasema ujumbe wao kwa wananchi huwa dhaifu.

“Wananchi hawahitaji kuona mapambano ya viongozi pekee, wanahitaji kuona mapambano ya mawazo, sera na suluhisho za matatizo yao,” anasema.

Anaeleza historia ya siasa inaonyesha kuwa vyama vinavyoweza kujenga umoja huwa na nafasi kubwa ya kushawishi wananchi kuliko vile vinavyogawanyika mara kwa mara.

Mfano wa ushirikiano wa vyama mbalimbali katika vipindi tofauti umeonyesha kuwa nguvu ya pamoja inaweza kuongeza ushawishi wa kisiasa.

“Umoja hauondoi tofauti, lakini unafanya tofauti hizo zitumike kujenga nguvu badala ya kuangamizana kisiasa,” anasema Dk Mtemi.

Kwa sasa, anasema changamoto kubwa kwa upinzani ni namna ya kutofautiana bila kuvunja msingi wa ushirikiano.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa sayansi ya siasa, Neema Kilango anasema migogoro inayoshuhudiwa ndani ya vyama vya upinzani inapaswa kutazamwa zaidi ya maneno ya viongozi.

Anaeleza ni suala linalogusa uwezo wa vyama hivyo kujenga taasisi imara na kuwa na mwelekeo unaoeleweka kwa wananchi.

“Chama cha siasa hakiwezi kuwa na nguvu kwa sababu kina viongozi wengi, kinakuwa na nguvu pale kinapokuwa na dira moja,” anasema.

Kwa miaka mingi, anasema vyama vya upinzani vimekuwa vikidai kuwa vina jukumu la kusimamia Serikali na kutetea maslahi ya wananchi.

Lakini, anasema migogoro ya ndani inapochukua nafasi kubwa, wananchi wanaweza kuona kama vyama hivyo vinapambana zaidi kwa maslahi yao binafsi.

“Wakati viongozi wanapigana hadharani, wananchi huanza kuuliza kama mapambano hayo yana maslahi yao au ni ya viongozi,” anaeleza.

Changamoto nyingine, anasema migogoro inaweza kuvunja matumaini ya wapigakura waliotaka kuona nguvu ya pamoja katika siasa.

Anasema wafuasi wengi huamini vyama vya upinzani vinaweza kuwa na ushawishi mkubwa zaidi vikishirikiana.

“Historia inaonyesha kuwa vyama vinapogawanyika bila sababu za msingi, mara nyingi hupoteza nguvu ya kisiasa,” anasema.

Схожие новости

#Наименование новостиТональностьИнформативностьДата публикации
1Masaju anavyoibua matarajio mhimili wa Mahakama01028-07-2026
2KONA YA MALOTO: Kumwelewa Nchimbi inatakiwa ung’amue alikoficha nukta01028-07-2026
3Safari ya Kanali Kipingu kunoa kizazi cha wasomi nchini01028-07-2026
4Sendiga ‘anavyowateka’ wananchi kwa kujifananisha nao01028-07-2026
5Zanzibar inaandika ukurasa mpya au inarudia historia?01028-07-2026
6Kauli 'leo lazima niue mtu' ilivyogeuka hukumu ya kifo01029-07-2026
7Завтра сон расскажет жителям Калмыкии об исполнении желаний013.4729-07-2026
8Tanzania: Power Infrastructure Vandalism Hits Muleba09.2629-07-2026
9Huyu hapa Miss Tanzania wa kwanza wa mwaka 1967017.7820-07-2026
10Simulizi ya Lipston na ndoto yake ilivyozima ghafla06.1717-07-2026

Классификация: Пресс-релизы. Схожих патентов: 0. Схожих новостей: 10. Тональность: 0. Информативность: 10. Источник: www.mwananchi.co.tz.